Shirika la CEFA lakamilisha rasmi shughuli zake Endough

Na Benson Aswani
Shule ya upili ya wasichana ya Kriich katika wadi ya Endough kaunti ya Pokot magharibi ni moja ya shule ambazo zimenufaika na miradi inayoendelezwa na shirika la CEFA.
Akizungumza wakati wa kufunga rasmi miradi ambayo shirika hilo limekuwa likiendeleza, meneja wa miradi Irene Sciurpa alisema miongoni mwa miradi ambayo imetekelezwa kuifaidi shule hiyo ni pamoja na kuhakikisha uwepo maji safi, upanzi wa miti, mboga pamoja na mradi wa mpunga.
Aliipongeza jamii ya eneo hilo kwa ushirikiano ambao walilipa shirika hilo hali ambayo alisema imesaidia pakubwa kuafikia malengo yake na kuhakikisha kwamba wanafunzi wa shule hiyo wanaendeleza shughuli za masomo katika mazingira salama.
“Hakukuwa na maji katika shule hii na hata kuna baadhi ya majengo ambayo hayakuwa yamekamilika. Tulianza kwa kuleta maji, kupanda miti, chakula na mambo mengine mengi ambayo tumetekeleza. Tunashukuru sana jamii ya eneo hili maana kama si wao hatungefika mahali tumefika sasa,” alisema Bi Sciurpa.
Kauli yake ilisisitizwa na afisa katika shirika hilo Beatrice Adeny ambaye aidha alisema hata shirika la CEFA linapokamilisha shughuli zake kwenye shule hiyo, wadau wanapasa kuhakikisha kwamba miradi hiyo inaendelea kuimarika ili kuwanufaisha wanafunzi na jamii.
“Tuweze kupiga jeki shule hii. Wapate walimu wengi, maafisa wa kilimo pamoja na wale wa mazingira ambao watakuwa wakiwatembelea na kuwafunza. Tukifanya hivyo sote, shule hii itafika mbali,” alisema Adeny.
Kwa upande wake afisa katika wizara ya kilimo kaunti ya Pokot magharibi Mathiews Lodomo alielezea kujitolea serikali ya kaunti kushirikiana na mashirika ya kijamii katika kuhakikisha kwamba maisha ya wakazi wa kaunti yanaimarika.
“Tumeshirikiana kikamilifu na shirika hili katika kuafikia malengo yake kwa jamii ya eneo hili, na kama serikali tupo tayari kushirikiana na shirika lolote ambalo nia yake ni kuimarisha maisha ya wakazi wa kaunti hii,” alisema Lodomo.
Naibu mwalimu mkuu wa shule hiyo Emmanuel Kakirokwo alipongeza shirika hilo kwa miradi ambayo limetekeleza aliyosema imekuwa ya manufaa makubwa kwa walimu na wanafunzi.