Kachapin aisuta idara ya elimu kwa kuendeleza ubaguzi

Na Benson Aswani,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin amelalamikia kile amedai kuendelezwa ubaguzi katika idara ya elimu, kaunti zingine zikipendelewa kuliko kaunti hii ya Pokot magharibi.


Akizungumza katika hafla moja Jumapili, gavana Kachapin alimsuta katibu katika wizara ya elimu Julius Bitok kwa kutoa ahadi ya shilingi milioni 10 kwa shule ya upili ya Ortum alipozuru shule hiyo juma lililopita, huku akitoa hundi ya shilingi milioni 200 katika kaunti ya Uasin Gishu.

“Haiwezekani kwa katibu wa elimu aje hapa Pokot magharibi aahidi shilingi milioni 10, lakini jioni iyo hiyo anapeana hundi ya shilingi milioni 200 kwa majirani zetu hapa. Haya ndio maswala yanayofanya kusiwe na usawa hapa nchini,” alisema Kachapin.


Kachapin aliitaka wizara ya elimu kuangazia jinsi ya kuendeleza usawa kwenye ufadhili wa sekta ya elimu kwa kaunti zote nchini ili sehemu zingine zisionekane kutengwa huku zingine zikinufaika.
Alisema japo lengo la kuanzishwa serikali za ugatuzi lilikuwa kuleta usawa nchini, sekta ya elimu imeendeleza ubaguzi wa wazi katika kusambaza raslimali.


“Ugatuzi umesaidia pakubwa kwa swala la usawa lakini tunataka wizara ya elimu ipangilie mambo yake vizuri. Si kwamba katibu wa elimu anakuja hapa kutoa ahadi tupu huku fedha zinatolewa kwa kaunti zingine,” alisema.


Akizungumza katika shule ya wavulana ya Ortum katika hafla ya mchango kwa ajili ya ujenzi wa miundo mbinu katika shule hiyo, Bitok aliahidi kuwasiliana na rais William Ruto ili kutengwa shilingi milioni 10 kwa ajili ya shule hiyo.