Serikali yatakiwa kuweka mikakati mwafaka kabla ya kurejelewa uchimbaji madini Pokot magharibi

Na Benson aswani,
Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameitaka serikali ya kitaifa kuweka mikakati ya usalama maeneo ya kuchimba migodi katika kaunti hiyo kabla ya kuruhusu shughuli hiyo kurejelewa rasmi.
Wakizungumza baada ya kuzuru eneo la Turkwel kutathmini hali tangu kusitishwa rasmi shughuli hiyo kwa wale wanaotumia mashine, viongozi hao wakiongozwa na mbunge wa Sigor Peter Lochakapong walipongeza hali kwamba tangu kusitishwa shughuli hiyo hamna maafa ambayo yameripotiwa.
Aidha viongozi hao walitoa wito kwa serikali kuwawezesha wakazi ambao wanaendeleza shughuli hiyo kwa kutumia vifaa vidogovidogo ambao walipewa idhini ya kuiendeleza, ili pia wawe salama wanapojitafutia riziki zao.
“Tumefurahi kwa sababu sasa zile mashine kubwa ambazo zimekuwa zikitumika kuchimba madini kaunti hii zimesimama. Sasa serikali iweke utaratibu ambao unafaa ili watu waweze kunufaika na shughuli hii ya uchimbaji madini,” alisema Lochakapong.
Kauli yake ilisisitizwa na mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto ambaye alipongeza hatua ya kusitishwa shughuli hiyo ambayo alisema kando na kusababisha maafa kwa wakazi ambao wanategemea dhahabu kujikimu kimaisha, ilichangia pakubwa uharibifu wa mazingira.
“Kile tulikataa ni zile mashine ambazo zilichimba hadi zikaanza kuleta maafa. Nashukuru serikali kwa sababu ilisimamisha shughuli hiyo ambayo ilikuwa pia ikiathiri mazingira,” alisema Moroto.