Serikali yangu ni safi kama pamba; Kachapin

Simon Kachapin Gavana wa kaunti ya Pokot Magharibi, Picha/Benson Aswani
Na Emmanuel Oyasi,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ametetea vikali utendakazi wa serikali yake akisema kwamba imezingatia pakubwa uadilifu katika matumizi ya fedha za umma.
Katika mahojiano na kituo hiki, Kachapin alisema kwamba visa vya matumizi mabaya ya fedha za umma havijashuhudiwa katika utawala wake tangu alipoanza kuwa gavana wa kwanza wa kaunti hiyo, na hata aliporejea kukamilisha muhula wake wa pili kama gavana.
Alisema yeye pamoja na maafisa wanaofanya kazi chini ya serikali yake wamehakikisha kwamba fedha ambazo zinatengewa miradi mbali mbali katika kaunti hiyo zinatekeleza na kufanikisha malengo yake.
“Hadi kufikia sasa tangu kipindi changu cha kwanza kama gavana, naweza kusema ya kwamba tumejaribu sana kujiepusha na maswala ya ufisadi. Pesa ambazo tunatenga tunahakikisha kwamba zinafanya kazi ambayo imekusudiwa,” alisema Gavana Kachapin.
Aidha gavana Kachapin alisema uchunguzi ambao umeendeshwa na idara mbali mbali za uchunguzi katika kipindi ambacho amehudumu kama gavana wa kaunti hiyo, umebaini kwamba serikali yake imezingatia pakubwa uadilifu katika matumizi ya fedha.
“Tumepea ruhusa vitengo vyote vya uchunguzi kuendesha uchunguzi wao, na wamehakikisha kwamba kazi inafanyika vizuri. Na mimi ninafurahi kwa sababu hakuna haja ya kupeana miradi hewa na unachukua fedha za umma. Hiyo ni laana,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kuonya maafisa ambao watajihusisha na ufisadi katika serikali yake kwamba watabeba msalaba wao wenyewe.
“Nimesema na ninarudia kwamba wale wanaofanya kazi nami wakijihusisha na ufisadi wenyewe watabeba msalaba wao. Hakuna mtu nimemshauri kuiba fedha za umma,” aliongeza.