Kachapin atofautiana na wanaopinga mwafaka baina ya Ruto na Raila

Simon Kachapin-Gavana Wa Kaunti Ya Pokot Magharibi,Picha/Benson Aswan

Na Emmanuel Oyasi,
Gavana wa kaunti ya Pokot magharibi Simon Kachapin ameunga mkono ushirikiano kati ya rais William Ruto na kinara wa chama ODM Raila Odinga ambao umepelekea kubuniwa serikali jumuishi inayohusisha viongozi kutoka chama cha ODM.


Akizungumza jumanne katika hafla moja ya mazishi eneo la Murkwijit, kachapin alisema kwamba hatua ya kujumuishwa viongozi wakuu kutoka chama cha ODM katika serikali ya Kenya kwanza ni muhimu katika kuimarisha utendakazi wa rais William Ruto.


“Tunaunga mkono kikamilifu serikali jumuishi ambayo imeundwa na rais William Ruto na kinara wa ODM Raila Odinga. Kile ninaomba ni kwamba tuunge mkono serikali hii ili itimize malengo yake kwa wananchi,” alisema Gavana Kachapin.


Gavana Kachapin alipigia upatu hatua ya kujumuishwa viongozi wa ODM serikalini aliosema wana utaalam ambao utasaidia pakubwa serikali ya rais Ruto kufanikisha malengo yake.


“Kwa hivyo sisi tunafurahia kujumuishwa viongozi wa ODM. Sasa wameungana, walete huo ujuzi wa ODM ili turekebishe yale maneno ambayo yanasumbua sisi Kenya,” alisema.

Aidha Gavana Kachapin alitoa wito kwa viongozi wanaoendeleza ukosoaji dhidi ya serikali ya rais William Ruto kuipa muda wa kutekeleza yale iliyowaahidi wananchi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliopita.


“Nafikiri ni wakati tunapasa kuacha kukosoa kila kitu ambacho kinafanywa na serikali ya rais Ruto. Tumpe muda wa kutosha atimize yale ambayo aliwaahidi wakenya. Iwapo kuna yale ambayo hatakuwa ametekeleza, kuna wakati mzuri wa kufanya uamuzi. Lakini kwa sasa tumpe muda,” aliongeza.


Kando na hayo Gavana Kachapin aliwahimiza viongozi wa kaunti hiyo kuendelea kushirikiana na kujitenga na siasa za vyama.


Alisema siasa za uchaguzi mkuu wa mwaka 2027 bado hazijachukua mkondo kutokana na hali kwamba vyama vingi vilivyokuwa pinzani sasa vinashirikiana katika serikali moja.