WANAFUNZI WASHAURIWA KUJIEPUSHA NA MIGOMO SHULENI.
Mkurugenzi wa elimu katika kaunti ya Pokot magharibi Simon Wamae amewahimiza wanafunzi kukoma kujihusisha na hulka ambazo huenda zikaharibu mali ya shule wakati wanapolalamikia maswala mbali mbali shuleni.
Akizungumza afisini mwake, Wamae alisema kwamba zipo njia bora ambazo wanafunzi wanaweza kutumia kuwasilisha malalamiko yao kwa idara husika, wanapohisi kutoridhika na huduma ambazo wanapokezwa na uongozi wa shule.
Wamae alisema mengi ya maswala ambayo wanayashinikiza wanafunzi wanapohisi kutoridhishwa yanaweza kushughulikiwa pasi na kuwalazimu wanafunzi kushiriki migomo na kuharibu mali ya shule.
“Zipo njia kadhaa ambazo wanafunzi wanaweza kutumia kuwasilisha malalamishi yao iwapo hawajaridhishwa na uongozi wa shule bila kushiriki maandamano na kuharibu mali ya shule. Mara nyingi mambo ambayo yanashinikizwa na wanafunzi yanaweza kushughulikiwa kwa urahisi sana.” Alisema Wamae.
Wakati uo huo Wamae alitoa wito kwa wazazi kuwa karibu na wanao na kuwashauri kila mara dhidi ya kushiriki migomo, kwani inapoteza muda ambao wangetumia kuendeleza masomo darasani, na kwamba ni wao watakaogharamika iwapo kutashuhudiwa uharibifu wakati wa migomo hiyo.
“Tunawashauri pia wazazi kuzungumza na wanao na kuwaeleza umuhimu wa masomo kwa sababu wanaposhiriki migomo wanapoteza muda wa kusoma. Na pia uharibifu ambao unasababishwa na migomo hiyo unagharamiwa na wazazi.” Alisema.