WAGOMBEA NYADHIFA KATIKA UCHAGUZI WA KNUT WAENDELEA KUJIPIGIA DEBE.

Wagombea wa viti mbali mbali katika chama cha walimu nchini KNUT kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kujipigia debe kuelekea uchaguzi wa viongozi wa chama hicho ambao umeratibiwa kuandaliwa tarehe 24 mwezi huu wa februari.

Mgombea wadhifa wa mwakilishi kina mama katika chama hicho Fridah Chemel aliahidi kuhakikisha kwamba haki za mwalimu wa kike zinazingatiwa katika taaluma ya ukufunzi ikiwemo kupewa uhamisho ambao huenda ukaleta mazingira tata kwa mwalimu wa kike.

Aidha Chemel alisema atapigania pakubwa haki za watoto ambao wanakabiliwa na maswala mengi katika kaunti hiyo hasa utovu wa usalama ambao umepelekea wengi wao kukosa kuhudhuria masomo vyema kama wenzao maeneo mengine ya nchi hali wanatathminiwa sawa katika mitihani ya kitaifa.

“Natafuta huu wadhifa kwa sababu kuna mambo ambayo nataka kufanya katika chama cha KNUT. Kwanza, kuhakikisha kwamba haki za walimu wa kike zinazingatiwa katika kutekeleza maswala mbali mbali ikiwemo uhamisho. Pia nataka kuhakikisha kwamba swala la usalama maeneo ya mipakani linaangaziwa kwa upana ili kuwapa nafasi watoto maeneo hayo kupata elimu.” Chemel.

Kwa upande wake mwaniaji wadhifa wa naibu katibu mkuu Rusikia Joseph alisema atahakikisha kwamba usalama wa walimu ambao wanahudumu katika maeneo yanayoshuhudia utovu wa usalama unapewa kipau mbele.

“Mara nyingi walimu wanaofunza katika shule za mipakani wanapitia changamoto kubwa sana kutokana na utovu wa usalama. Nikipewa nafasi hii nitahakikisha kwamba serikali ya kaunti inashirikiana na serikali kuu kuhakikisha  walimu hawa wanapata usalama wa kutosha.” Alisema Rusikia.