KOMOLE AAPA KUTONYAMAZISHWA NA MAAGIZO YA KUANDIKISHA TAARIFA NA DCI KUHUSU USALAMA BONDE LA KERIO.

Naibu gavana kaunti ya Pokot magharibi Robert Komole.

Na Emmanuel Oyasi.

Naibu gavana kaunti ya Pokot magharibi Robert Komole ameshutumu hatua ya kuagizwa kuandikisha taarifa katika makao makuu ya DCI mjini Nakuru wiki jana kufuatia swala zima la utovu wa usalama mipakani pa kaunti hiyo.

Komole alisema kwamba kamwe hatua hiyo haitawafanya viongozi katika kaunti hiyo kukoma kuzungumzia swala hilo hadi serikali kupitia wizara ya usalama itakapokabili swala la utovu wa usalama na kuhakikishia wakazi wa kaunti hiyo usalama wao.

Alimsuta waziri wa usalama na maswala ya ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki kwa kile alidai kuwahangaisha viongozi wa kaunti hiyo.

Aidha Komole alimtaka waziri Kindiki kufika katika eneo la bonde la kerio na kuandaa mkutano wa viongozi wa kaunti zote za bonde la kerio ili kutafuta suluhu kwa tatizo la utovu wa usalama badala ya kuketi afisini na kutoa maagizo ya kukamatwa viongozi.

“Nataka nimwambie waziri wa usalama Kithure Kindiki kwamba asidhani sisi tutanyamaza kuhusu swala la utovu wa usalama kwa kutuita tuandikishe taarifa na DCI. Tutaendelea kuongea hadi swala la utovu wa usalama litakapokabiliwa.” Alisema Komole.

Yanajiri haya huku mbunge wa Kapenguria Samwel Moroto na mwenzake wa Kacheliba Titus Lotee wakitarajiwa kufika katika makao makuu ya DCI mjini Nakuru, kuandikisha taarifa kuhusiana na madai ya uchochezi na misururu ya visa vya utovu wa usalama kwenye eneo la kaskazini mwa bonde la ufa.

“Nimeagizwa mimi na mbunge wa Kacheliba Titus Lotee kufika katika makao makuu ya DCI huko Nakuru kuandikisha taarifa kuhusiana na swala la utovu wa usalama eneo hili. Nashangaa ni vipi tunaeneza uchochezi wakati tumekuwa msitari wa mbele kuhimiza amani.” Alisema Moroto.