ZIARA YA KINDIKI BONDE LA KERIO YATAJWA KUWA MUHIMU KATIKA MCHAKATO WA KULETA AMANI.

Viongozi kaunti ya Pokot magharibi wamepongeza ziara za waziri wa usalama na maswala ya ndani ya nchi Prof. Kithure Kindiki alizofanya katika kaunti za bonde la kerio mwishoni mwa juma lililopita.

Akizungumza na wanahabari kuhusiana na ziara hiyo naibu gavana kaunti ya Pokot magharibi Robert Komole alisema kwamba hatua hii ya waziri Kindiki ni muhimu zaidi katika kuimarisha vita dhidi ya utovu wa usalama ambao umeshuhudiwa kwa muda katika kaunti hizi.

Komole alisema fursa hii ya kukutana na waziri wa usalama ilikuwa imesubiriwa kwa muda na viongozi wa kaunti hiyo, ili kumweleza hali halisi ilivyo na jinsi ya kushirikiana na viongozi wa kanda hii katika kukabiliana na wahalifu wanaotekeleza uvamizi wa kila mara.

Alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa waziri Kindiki kuzuru maeneo haya kwa wingi ili kuwaleta pamoja viongozi wa kaunti hizi katika juhudi za kuafikia amani.

“Tunamshukuru waziri wa usalama Kithure Kindiki kwa kutenga muda wa kuzuru kaunti za bonde la kerio juma lililopita ili kuangazia jinsi hali ilivyo kutokana na usalama. Tunalomwomba ni kwamba atembelee eneo hili kwa wingi ili watu wetu waweze kutangamana.” Alisema Komole.

Wakati uo huo Komole alisema kama viongozi wanaunga mkono kikamilifu shughuli ya kuondoa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria miongoni mwa raia ila akamtaka waziri Kindiki kuwashauri maafisa wanaoendeleza shughuli hiyo kuwa na uhusiano mwema na viongozi pamoja na watawala wa maeneo haya ili wapate habari kamilifu kuhusu silaha hizi.

“Kama viongozi tukiongozwa na gavana wetu tunaunga mkono swala la kuondoa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria miongoni mwa raia. Wale ambao wanafanya shughuli hiyo tunaomba kwamba washirikiane na viongozi pamoja na watawala wa kaunti hizi ili wapate habari zitakazosaidia kufanikisha shughuli hii.” Alisema.