ZAIDI YA WATU 1000 WAKABILIWA NA MATATIZO YA AKILI TRANS NZOIA.

Serikali ya Kaunti ya Trans Nzoia imeweka mikakati ya kuimarisha matibabu kwa watu wanaoishi na matatizo ya akili.

Akihutubu kwenye hafla ya maadhimisho ya siku ya afya ya akili ulimwenguni mkurugenzi wa  afya Kaunti ya Trans Nzoia Nancy Kegode amesema zaidi ya watu Milioni 792 wanakabiliwa na matatizo ya akili huku  11% wakiwa wanawake na 9.3% wakiwa ni  wanaume.

Kegode ametaja msongo wa mawazo na matumizi ya dawa za kulevya  kuwa vyanzo vikuu vinavyosababisha matatizo ya akili. 

“Hii leo nchini Kenya mtu mmoja kati ya wanne wanaotafuta huduma za afya ana matatizo ya akili. Katika hospitali ya kaunti ya Kitale kuna wagonjwa alfu 1,167 ambao wanapata huduma za kiakili na kati ya hao 705 ni visa vipya.” Alisema.

Kwa upande wake Msimamizi mkuu wa matibabu katika Hospitali ya Rufaa mjini Kitale Dr. Francis Soita amesema afya ya akili ni kiungo muhimu kwa binadamu na serikali ya Kaunti ya Trans Nzoia imeweka mikakati kuhakikisha utoaji wa huduma bora  ya afya ya akili kwa walio na matatizo hayo.

“Afya ya akili ni muhimu sana katika maisha yetu. Sasa tupo hapa kusherehekea siku hii na tuna kundi la watu waliojitolea kuhakikisha kuwa wale ambao wana matatizo ya akili wanapata huduma bora ili pia waweze kuwa na wakati mwema.” Alisema Soita.