ZAIDI YA WANAFUNZI ALFU 7 WAREJESHWA SHULENI POKOT MAGHARIBI KUFUATIA USHIRIKIANO KATI YA IDARA YA ELIMU NA MASHIRIKA YA KIJAMII.
Zaidi ya wanafunzi alfu 7 ambao walikuwa wameacha masomo wamerejeshwa shuleni kufuatia harakati za kuwarejesha shuleni wanafunzi hao, ambazo zinaendelezwa na idara ya elimu kwa ushirikiano na mashirika mbali mbali ya kijamii.
Haya ni kwa mujibu wa mkurugenzi wa elimu kaunti hii ya Pokot magharibi Simon Wamae ambaye alisema kwamba kando na msaada wa mashirika ya kijamii juhudi hizi zimefanikiwa pia kufuatia ushirikiano ambao umekuwepo baina ya walimu wakuu, machifu na idara nyingine za usalama.
Wamae alisema hali ya wazazi kuhamahama katika juhudi za kutafuta lishe kwa ajili ya mifugo yao ndicho chanzo kikuu cha idadi kubwa ya wanafunzi kuacha masomo, akitoa hakikisho kwamba mikakati ambayo imewekwa itapelekea hali hii kukomeshwa.
“Hadi sasa tumejaribu hapa kwetu kupitia idara ya elimu kuwarejesha shuleni watoto alfu 7,094. Tuna mashirika mbali mbali ambayo yamesaidia katika juhudi hizi. Kando na mashirika haya, ushirikiano baina ya wakuu wa shule mbali mbali na machifu pamoja na idara za usalama umepelekea kuafikia malengo.” Alisema Wamae.
Wakati uo huo Wamae alitoa hakikisho la masomo kuendelea vyema maeneo mbali mbali ya kaunti hiyo ya Pokot magharibi isipokuwa shule moja eneo la Turkwel ambayo ililazimika kufungwa kufuatia hali ya usalama, ili kutoa nafasi kwa wadau kuweka mikakati ya kuhakikisha usalama wa wanafunzi.
“Shule zetu nyingi zinaendelea vyema, isipokuwa shule moja eneo la Turkwel ambako kulikuwa na uhasama kati ya jamii mbili, tukaona kwamba msuko suko huu unaweza kuwadhuduru wanafunzi na ndipo tukasema shule hiyo ifungwe, ili wadau waweke mikakati ya kuhakikisha kwamba wanafunzi wanasalia salama.” Alisema.