ZAIDI YA MAAFISA 216 WA NPR WASAJILIWA KATIKA JUHUDI ZA KUIMARISHA USALAMA BONDE LA KERIO.


Naibu kaunti kamishna eneo bunge la marakwet mashariki kaunti ya Elgeiyo marakwet Simon Osumba amesema tayari maafisa wa akiba NPR wapatao 216 wamesajiliwa kama alivyoagiza waziri wa usalama wa ndani prof. Kithure kindiki.
Akiongea baada ya kuwaelekeza maafisa hao katika maeneo yao ya kuhudumu, Kindiki alisema kuwa usajili wa maafisa hao unalenga kuipa nguvu idara ya usalama katika kudumisha amani kwenye bonde la kerio.
“Waziri wa usalama wa ndani ya nchini Prof. Kithure Kindiki alituagiza kuhakikisha kwamba maafisa wa akiba NPR wanasajiliwa kusaidia katika kuimarisha usalama eneo hili la bonde la kerio. Tunavyojua hali ya usalama imekuwa tete sana kanda hii na tunaamini maafisa hawa watasaidia pakubwa kukabiliana na wahalifu hawa.” Alisema Osumba.
Osumba aliongeza kwa kusema, “hadi kufikia sasa tumewasajili maafisa wa NPR wapatao 216 na ambao ni wakazi wa maeneo haya wanaofahamu kila kona sehemu hii na tunaamini watakuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha usalama.”
Osumba aidha aliwataka wakazi kushirikiana na maafisa hao wa polisi wa akiba ili kuiwezesha serikali kukabili tatizo la wizi wa mifugo ambalo limepelekea utovu wa usalama kwenye baadhi ya maeneo ya kaunti za kaskazini mwa bonde la ufa.
“Natoa wito kwa wakazi wa maeneo haya kushirikiana kwa ukamilifu na hawa vijana wetu wa NPR ambao sasa tumewachukua rasmi ili wasaidie kudumisha usalama na tunahakikisha kwamba mifugo sasa watakuwa na walinzi wanapokwenda malishoni.” Alisema.
Osumba alisema kwamba zoezi la kuwasajili maafisa hao litaendelea hadi watakaposajiliwa jumla ya maafisa 300 wa NPR katika juhudi za kuimarisha usalama eneo zima la bonde la Kerio.