World Vision laikabidhi rasmi serikali ya kaunti ya Pokot Magharibi soko la mifugo la Orolwo

Na Emmanuel Oyasi,
Wakulima wa mifugo katika eneo la Orolwo wadi ya Kodich katika kaunti ya Pokot magharibi wamepata afueni baada ya shirika la World Vision kukabidhi rasmi soko la mifugo la Orolwo kwa serikali ya kaunti tayari kwa matumizi.
Akizungumza katika hafla hiyo, meneja wa shirika hilo Moses Kiptugen alisema, soko hilo ambalo liligharimu kima cha shilingi milioni 15 kwa ufadhili wa serikali ya Uswidi, limegawanywa kwenye vitengo mbali mbali kulingana na aina ya mifugo ambao watakuwa wakiuzwa.
Aliwahimiza wakazi wa eneo la Orolwo na maeneo ya karibu kutumia vyema soko hilo katika kuuza mifugo yao ili kuweza kunufaika na shughuli zao za kilimo cha ufugaji.
“Mradi huu unajumuisha kitengo ambapo wanyama wadogo kama mbuzi na kondoo wanawekwa na sehemu ya wanyama wakubwa kama ngamia na ng’ombe. Kwa hivyo nawahimiza sana wakazi wa eneo hili kutumia soko hili ili waweze kunufaika zaidi kwa mifugo wao,” alisema Kiptugen.
Akipokea mradi huo kwa niaba ya gavana, waziri wa biashara, mashirika, viwanda na kawi Joshua Ruto amelipongeza shirika hilo kwa mradi huo aliosema utasaidia pakubwa katika kuimarisha biashara ya mifugo eneo hilo na kukuza uchumi wa wakazi na kaunti kwa ujumla.
“Tunashukuru sana shirika la World Vision kwa kazi nzuri ambayo wanafanya katika kaunti hii. Mradi huu ni mkubwa sana ambao unaweza kuwafaidi watu wa Orolwo, si wafanyibiashara wa mifugo pekee bali pia wafanyibiashara wadogo wadogo kama wale wa kuuza chakula,” alisema Ruto.