WIZI WA NG’OMBE WATEKELEZWA KAPEDO NA KAKAMEGA


Mtu mmoja anahofiwa kufariki huku mwingine akijeruhiwa vibaya baada ya wezi wa mifugo kudaiwa kuvamia kijiji kimoja katika eneo la Kapedo mpakani pa kaunti za Baringo na Turkana.
Inaarifiwa kuwa wanafunzi wa shule ya wavulana ya Kapedo wamehamishwa kwenye maeneo salama kwenye vijiji tofauti.
Hata hivyo Polisi wameimarisha doria sehemu hiyo ili kuhakikisha kuwa hakuna tukio lingine linalotokea kwa sasa.
Hayo yanajiri huku ng’ombe mmoja akiripotiwa kuibwa usiku wa kuamkia leo kutoka kwa boma la mkaazi mmoja wa kijiji cha msalaba Yellow kwenye eneo bunge la Likuyani.
Inaarifiwa kuwa washukiwa walimuiba ng’ombe huyo kisha kumchinja katika shamba moja katika eneo bunge la Soy kwewnye kaunti ya Uasin Gishu.
Akizungumza na wanahabari mwathiriwa Haman Kibilia amesema kuwa baada ya kukosa ng’ombe wake zizini alianza kumsaka kabla ya kupata miguu yake, kichwa na hata ngozi shambani.
Kibilia aidha ametoa wito kwa idara ya usalama kuimarishwa doria hasaa nyakati za usiku akisema kuwa wezi wengi hupenda kutekeleza uhalifu wakati huo.
Akithibitisha kisa hicho chifu wa Soy Augustine Kiprono amesema kuwa hiki ni kisa cha nne kuripotiwa huku akisema kuwa tayari uchunguzi umeanzishwa kuwasaka washukiwa.