WIZARA YA USALAMA YATAKIWA KUHARAKISHA MCHAKATO WA KUWAAJIRI MAAFISA WA NPR.
Mwakilishi wadi ya seker kaunti ya Pokot magharibi Jane Mengich ameitaka wizara ya usalama na maswala ya ndani ya nchi kuharakisha mchakato wa kuhakikisha maafisa wa akiba NPR wanaanza kuhudumu hasa maeneo ambayo yanakabiliwa na utovu wa usalama kaunti hiyo.
Akizungumza katika hospitali ya Kapenguria alipowatembelea waathiriwa wa bomu ambalo linaaminika kurushwa na maafisa wa KDF ambapo watu watatu walifariki dunia eneo la Lochacha, Mengich alisema kwamba wahalifu wamezidisha uvamizi maeneo hayo punde tu baada ya kutangazwa mchakato wa kuwaajiri maafisa wa NPR katika kaunti hiyo.
Aidha Mengich alimtaka waziri wa ulinzi Aden Duale kuzuru eneo hilo na kutathmini shughuli za maafisa wa KDF ikizingatiwa wanahudumu chini ya wizara yake.
“Huu uvamizi ulipofanyika, watu wetu walijaribu kukabiliana nao lakini maafisa wa KDF wakaingilia kati na kurusha bomu na kuwaua watu wetu. Ni kama wahalifu hawa wanashirikiana na maafisa wa KDF walio eneo la Kainuk.” Alidai Mengich.
Wakati uo huo Mengich alilaumu kituo cha polisi cha Lami nyeusi kwa kile alisema hakijakuwa na msaada wowote kwa wakazi wa maeneo hayo kutokana na madai ya kukosa raslimali za kuwawezesha kufanya doria na kuwakabili wahalifu wanaoendeleza uvamizi.
“Kuna kambi ya polisi ilijengwa pale lami nyeusi, askari wako kwenye kambi hiyo lakini hawana msaada wowote kwa wananchi wa eneo hilo. Uvamizi ukitokea hawashughuliki, na ukijaribu kuwaita wanasema hawana mafuta kwenye magari yao.” Alisema.