WIZARA YA USALAMA YATAKIWA KUBADILI MBINU YA KUWAKABILI WEZI WA MIFUGO BONDE LA KERIO.
Pana haja ya serikali kuu kupitia wizara ya usalama wa ndani kubadilisha mbinu ya kuwakabili wezi wa mifugo ambao licha ya oparesheni inayoendelea kwenye kaunti sita za bonde la ufa wameendelea kutekeleza uvamizi na mauaji.
Gavana wa kaunti ya Baringo Benjamin Cheboi akizungumza na waandishi wa habari alisema tishio kutoka kwa majangili limewafanya wakazi kuingiwa na hofu hadi kushindwa kujiendeleza kimaisha.
Gavana cheboi alisisitiza kwamba serikali inafaa itekeleze ahadi yake ya kuwakabili majangili hao haraka iwezekanavyo na kurejesha amani katika eneo la kerio valley na maeneo mengine nchini.
“Mara kwa mara serikali imekuwa ikisema kwamba tutawamaliza hawa watu ili waweze kuwaachilia watu kufanya shughuli zao, laikini hatujaona ikionyesha juhudi za kumaliza tatizo hili. Kwa sasa wakazi wa maeneo haya hawajafanya lolote ikizingatiwa huu ni msimu wa upanzi. Serikali inapasa kubadilisha mbinu ya kushughuli tatizo hili, na kutekeleza inachosema.” Alisema Cheboi.
Cheboi aliongeza kwamba wakazi wanafaa kuhakikishiwa uwepo wa usalama wa kutosha ili kuweza kutekeleza majukumu yao ipasavyo na kuhakikisha kwamba wanao wanapata masomo bila kutatizwa na utovu wa usalama.
“Usalama wa watu ni muhimu sana. Tunahitaji watu wetu wawe na usalama wa kutosha ili waweze kutekeleza shughuli zao za kilimo na kufuga mifugo wao wakiwa na uhakikisho wa usalama. La muhimu zaidi wanapasa kupata muda wa kufanya wawezalo ili wawe katika nafasi bora ya kuwaelimisha wanao.” Alisema.