WIZARA YA USALAMA YAANGAZIA UPYA MAKATAA YA WAKAZI KUONDOKA MAENEO YALIYOTAJWA KUWA MAFICHO YA WAHALIFU.
Wizara ya maswala ya ndani ya nchi imeangazia upya makataa ya saa 24 kuwataka watu wanaoishi kwenye maeneo 27 yanayoaminika kuwa maficho ya wezi wa mifugo kuondoka wakati huu ambapo makataa hayo yamekamilika.
Katika taarifa mpya waziri Kithure Kindiki aliondoa katika orodha hiyo mapango ya Turkwel na Ombolion kwenye kaunti za Pokot magharibi na Turkana, maeneo ya Kapelbok, Nakwamoru, Lokoron na Lobokat kwenye orodha ya maeneo ambayo wakazi wanatakiwa kuondoka.
Badala yake Kindiki aliwashauri wakazi wa maeneo hayo kuendelea na shughuli zao za kawaida kwa vile oparesheni hiyo haitayalenga maeneo hayo.
Akitoa agizo la kuwataka wakazi kuondoka maeneo hayo siku ya jumapili, waziri Kindiki alisema kwamba yeyote atakayepatikana kwenye maeneo hayo baada ya kukamilika makataa hayo atachukuliwa kuwa mhalifu na atakabiliwa na maafisa wa usalama wanaoendeleza oparesheni hiyo.
Tayari mamia ya ya wakazi kwenye maeneo ambayo yalitajwa kuwahifadhi wezi wa mifugo wameanza kuhama.
Baadhi waliozungumza na vyombo vya habari walitaka serikali kufanya kila juhudi kukabili utovu wa usalama kwa kutokomeza wizi wa mifugo huku wengine wakidai serikali inapasa kuwatafutia mahali pa kwenda.
Chama cha wanasheria nchini LSK kimekosoa makataa hayo ya saa 24 yaliyotolewa kwa wakazi kuhama.
Kulingana na rais wa LSK Eric Theuri serikali haiwezi kuwaagiza wakazi kuondoka maeneo yao bila ya kuwapa makazi mbadala.
Badala yake LSK ilitaja hatua hiyo kuwa inayowakandamiza wananchi wa maeneo husika.
Kauli kama hiyo ilitolewa na baraza la wazee wa jamii ya Turkana.
Kulingana na mmoja wa wanachama Abraham Lukuwoma, wakazi wa maeneo hayo hatari wameathirika pakubwa kufuatia kiangazi na njaa na hawafai tena kuongezewa mzigo mwingine wa kuwa wakimbizi.