WIZARA YA ELIMU YATAKIWA KUWEKEZA ZAIDI KATIKA MASWALA YA ELIMU KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI


Mbunge wa Kapenguria katika kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Moroto ameitaka wizara ya elimu kuwekeza zaidi katika shule za maeneo ya mashinani ili kuwapa nafasi wanafunzi katika shule hizo kupata huduma kama wanafunzi wengine.
Akizungumza katika shule ya upili ya mseto ya Tomena, Moroto amesema kuwa wanafunzi katika shule hizo wana mahitaji mengi ambayo yanafaa kushughulikiwa hasa ikizingatiwa hali ya chini ya kiuchumi ya wazazi wa wanafunzi hao.

Moroto amesema kuwa kwa ushirikiano na wadau mbali mbali wanapanga kujenga mabweni ya muda kwa ajili ya shule hasa za maeneo ya mashinani kuwakimu wanafunzi hasa wa kidato cha nne ili kuwapa muda bora kwa shughuli za masomo na kukabili changamoto wanazokumbana nazo nyumbani.

Wakati uo huo Moroto amepongeza kamati za shule eneo bunge hili kwa uwazi katika matumizi ya fedha ambazo zimekuwa zikitolewa na hazina ya CDF hali ambayo imepelekea eneo bunge hili kuorodheshwa miongoni mwa maeneo bunge ambayo yametumia vyema fedha za CDF.