WIZARA YA ELIMU POKOT MAGHARIBI YATARAJIWA KUFANYIA UCHUNGUZI SHULE YA UPILI YA CHEPKORNISWO KUFUATIA MAANDAMANO YA WANAFUNZI.


Waziri wa elimu kaunti ya Pokot magharibi Rebecca Lotuliatum amelalamikia kisa cha wanafunzi wa shule ya upili ya Chepkorniswo eneo la pokot kusini kuandamana hadi afisi za kaunti mjini Kapenguria kulalamikia uongozi wa shule hiyo.
Lotuliatum alisema kwamba inasikitisha kuona shughuli za masomo kwa wanafunzi zikitatizika hali ni majuzi tu ambapo serikali ya kaunti ilitoa fedha za basari kwa ajili ya wanafunzi hao kusalia shuleni kuendelea na shughuli zao za masomo.
Lotuliatum alisisitiza kwamba uchunguzi utaendeshwa kuhusiana na madai yaliyoibuliwa na wanafunzi hao na hatua kuchukuliwa iwapo kutapatikana utepetevu katika uongozi wa shule hiyo anliyosema kwamba imedorora kimatokeo katika miaka ya hivi karibuni.
“Nasikitika kwamba ni majuzi tu ambapo serikali ya kaunti imetoa basari kwa wanafunzi na sasa wamepoteza muda ambao wangekuwa darasani kwa kutembea kutoka Chepareria hadi kwenye afisi za kaunti. Tutafanya uchungzuzi wetu na kuchukua hatua tutakapopata tatizo linalowafanya wanafunzi hao kuandamana.” Alisema Lotuliatum.
Wakati uo huo Lotuliatum alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa viongozi wa kisiasa katika kaunti ya Pokot magharibi kutoingiza siasa kwenye taasisi za elimu na badala yake kuwapa nafasi walimu kutekeleza shughuli zao bila miingilio.
“Nawasihi wanasioa kutoingiza siasa katika taasisi za elimu na badala yake kuwapa walimu wakati wa kutekeleza shughuli zao za kuwahudumia wanafunzi. Siasa zikiingizwa kwenye shule basi masomo yataathirika pakubwa.” Alisema.
Mapema jumatatu wanafunzi kutoka shule ya Chepkorniswo waliandamana hadi afisi za kaunti mjini Kapenguria wakilalamikia uongozi wa shule hiyo huku wakishinikiza kupewa uhamisho mwalimu mkuu kwa kile walidai matumizi mabaya ya afisi.