WIZARA YA AFYA YAONDOA HOFU YA UWEPO WA UGONJWA WA KIPINDUPINDU POKOT MAGHARIBI.


Wizara ya afya katika kaunti hii ya Pokot magharibi imeondoa wasi wasi wa uwezekano wa kuzuka ugonjwa wa kipindu pindu katika kaunti hii baada ya kuibuka madai kuwa mgonjwa mmoja anatibiwa katika hospitali ya Kapenguria baada ya kupatikana na ugonjwa huo.
Waziri wa afya kaunti hii Cleah Parklea alisema kwamba mtu aliyekuwa akishukiwa kuwa na ugonjwa huo alifanyiwa vipimo na kubainika kwamba hakuwa anaugua kipindupindu na kwamba huenda ni chakula alichokula ndicho kilisababisha kuanza kuendesha na kuumwa na tumbo.
Aidha Parklea alisema zaidi ya watu 30 walioonyesha dalili hizo wamepimwa na kubainika hamna hata kisa kimoja cha ugonjwa wa kipindupindu ambacho kimeripotiwa.
“Kulikuwa na mtu ambaye alishukiwa kuwa na ugonjwa wa kipindupindu ila tukachukua hatua za haraka kumtenga na kumfanyia vipimo. Habari njema ni kwamba matokeo yalionyesha kuwa haukuwa na ugonjwa huo. Tunashuku huenda alipata maumivu ya tumbo na kuendesha kutokana na chakula alichokula kulingana na maelezo yake.” Alisema Parklea.
Aliongeza kuwa, “kufikia sasa tumefanyia vipimo zaidi ya watu 30 ambao wamekuwa wakionyesha dalili za ugonjwa huo ila hamna hata kisa kimoja ambacho kimethibitishwa.”
Parklea alitumia fursa hiyo kuwahimiza wakazi wa kaunti hii kuendelea kudumisha usafi kwa kuhakikisha kwamba wananawa mikono kila mara ili kuzuia mlipuko wa ugonjwa huo ambao umeripotiwa katika baadhi ya kaunti nchini.
“Nawahimiza wananchi wazingatie usafi pakubwa jinsi ilivyokuwa katika kipindi cha corona. Wanawe mikono kila wakati wanapotoka msalani na zaidi wahakikishe wanakunywa maji safi ili tuzuie mlipuko wa ugonjwa huo.” Alisema Parklea.