WITO WATOLEWA KWA MAAFISA WA POLISI KUFANYA UCHUNGUZI KUHUSIANA NA UVAMIZI ULIOSHUHUDIWA ENEO LA KAINUK KITALE LODWAR

Viongozi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wameendelea kulaani kisa ambapo gari moja lililokuwa likisafiri kutoka Lodwar kaunti ya Turkana kueleka Kitale lilidaiwa kumiminiwa risasi na watu wanaoaminika kuwa wavamizi.
Wa hivi punde kulaani kisa hicho ni seneta wa kaunti hii Samwel Poghisio ambaye ameelezea kusikitishwa na hali kuwa licha ya juhudi za kuhakikisha usalama unadumishwa maeneo haya visa hivi vinaendelea kuripotiwa.
Aidha Poghisio ametaka kutohusishwa jamii yoyote na visa kama hivi akisema kuwa wanaotekeleza uvamizi wowote ni wahalifu wanaofaa kukabiliwa vilivyo wala hawapasi kuhusishwa na jamii fulani.
Wakati uo huo Poghisio amewataka maafisa wa usalama kuwa macho zaidi ili kukabili jaribio lolote la uvamizi dhidi ya magari yanayotumia barabara hiyo na kuwahakikishia wakazi pamoja na wasafiri usalama wa kutosha.