WITO UMETOLEWA KWA TUME HURU YA UCHAGUZI IEBC KAUNTI YA POKOT MAGHARIBI KUENDESHA UCHAGUZI KWA UWAZI

Mwaniaji ugavana kaunti hii ya Pokot magharibi kupitia chama cha UDA Simon Kachapin amewasuta wapinzani wake wa kisiasa kwa kile amedai kutoa matamshi yanayoashiria kuwa watashirikiana na tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC kuiba kura.

Kachapin ambaye anawania tena kiti hicho baada ya kuhudumu kama gavana wa kwanza kaunti hii amesema kuwa IEBC ni tume huru inayotekeleza majukumu yake kwa uwazi na ni hatia kwa kiongozi yeyote kudai kuwa atainunua ili kumpendelea.

Amesema kuwa madai hayo ya wapinzani wake ni ishara kwamba wamehofia watashindwa naye katika uchaguzi mkuu wa mwezi agosti akisisitiza madai kama haya kamwe hayampi wasiwasi kuhusiiana na uchaguzi huo.

Wakati uo huo Kachapin ameendeleza shutuma zake kwa gavana wa sasa John Lonyangapuo kwa kile amedai kutotekeleza majukumu yake kwa njia inayoistahili hasa katika ugavi wa fedha za basari kwa wanafunzi licha kuongezeka pakubwa fedha zinazotengewa kaunti hii ikilinganishwa na wakati wake.