WILLIAM RUTO ATANGAZWA RAIS WA TANO WA KENYA.


Hatimaye naibu rais William Ruto aliyewania urais kupitia chama cha UDA ametangazwa rasmi rais mteule wa taifa hili la Kenya.
Akitangaza rasmi matokeo hayo mwenyekiti wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC Wafula Chebukati alisema Ruto aliibuka mshindi katika kinyang’anyiro hicho kwa kuzoa jumla ya kura milioni 7,176,141 ambayo ni asilimia 50.49, dhidi ya zile za mpinzani wake mwaniaji wa chama cha azimio la umoja one Kenya Raila Odinga aliyejizolea milioni 6,942,930 ambayo ni asilimia 48.85.
Chebukati alitumia uwezo wake wa kisheria kumtangaza rasmi Ruto kuwa rais wa tano wa taifa hili tangu Kenya kupata uhuru.
Chebukati alisema kuwa licha ya changamoto mbali mbali ambazo makamishina wa tume hiyo walipitia walihakikisha kuwa wakenya wanapata uchaguzi ulio huru na wa haki.
Aliwapongeza wadau wote walioshirikiana na tume hiyo kuhakikisha kuwa shughuli hiyo inakamilika kwa njia ya amani.
Punde baada ya tangazo hilo sherehe zilitanda kote mjini makutano katika kaunti hii ya Pokot magharibi.