WEZI WA MIFUGO WAENDELEA KUKAIDI OPARESHENI YA KIUSALAMA BONDE LA KERIO, HUKU IDADI YA NG’OMBE ISIYOJULIKANA WAKIIBWA TAMBACH.
Taharuki ingali imetanda katika kijiji cha Kapushen wadi ya Tambach eneo la pokot kusini kaunti ya Pokot magharibi baada ya wezi wa mifugo kuvamia eneo hilo usiku wa kuamkia jumapili na kuiba idadi ya mifugo isiyojulikana.
Mwakilishi wadi wa eneo hilo Samuel Timtim alilaani vikali kisa hicho na kuitataka serikali kufanya hima kurejesha mifugo hao huku akisuta maafisa wa usalama wa eneo la Kamelei kwa kile alisema kutomakinika katika kuhakikisha usalama wa wakazi wa eneo hilo.
“Ng’ombe wameibwa hapa Kamelei, na tunataka maafisa wa usalama kufanya hima kurejesha ng’ombe hao kabla hawajapelekwa mbali. Tuna kituo cha polisi hapa lakini hawashughuliki. Kwa sasa wako kituoni na ng’ombe wamechukuliwa.” Alisema Timtim.
Akithibitisha kisa hicho kwa njia ya simu inspekta wa polisi eneo hilo Aston Kambi alisema vyombo vya usalama viko mbioni kufuatilia tukio hilo huku akiahidi kuhakikisha kwamba mifugo hao walioibwa wanarejeshwa.
“Kuna ng’ombe watano ambao wameibwa na haijajulikana ni wakati gani walichukuliwa. Mwenye ng’ombe alikuja kwetu kuripoti asubuhi. Ila tunajaribu kufuatialia na tutafanya kila juhudi kuhakikisha kwamba ng’ombe hao wanarejeshwa.” Alisema Kambi.
Tukio hili lilijiri siku moja tu baada ya mifugo wengine kuibwa kaunti ya samburu huku maafisa wa usalama wakijeruhiwa kutokana na wizi huo.