WENYEJI WA KAUNTI HII YA POKOT MAGHARIBI WAMEBAKI NA MASWALI ALIKO GAVANA LONYANG’APUO


Ni muda wa wiki tatu saa tangu gavana wa kaunti hii ya Pokot Magharibi Prof John Krop Lonyang’apuo hajaonekana kwa umma baada ya kudaiwa kwamba alikuwa afisini mwake mara ya mwisho 17,Disemba,2020 nakwamba simu zake zote zimezimwa.
Hali hiyo imepelekea wenyeji wa kaunti hii kuwa na maswali chungu nzima.
Kaunti hii sasa inasemekana kuwa na pengo la uongozi kwa sababu naibu wa gavana kwenye kaunti hii Dkt Nicholas Atudonyang hajakuwepo kwa muda wa miaka mitatu sasa .
Dkt Atudonyang ambaye ni daktari wa kupasua akili ,anaishi nchini Texas, Marekani na amekuwa na tofauti na mkubwa wake Prof Lonyangapuo.
Kwa upande mwingine ,karani wa kaunti hii Dkt Mike Parklea pia hayupo baada ya kusimamishwa kazi kutokana na madai ya ufisadi.
Madai yameibuka kuwa ,gavana Lonyangapuo huenda ni mgonjwa lakini hakuna afisa yeyote wa serikali ya Pokot Magharibi amejitokeza kuelezea umma kuhusu hali ya kiafya ya gavana huyo.
Kwenye mahojiano ya kipekee ndani ya Mpigo wa Kalya Radio kaimu karani wa kaunti hii John Karamunya amedinda kuzungumza na badala yake kukata simu kwa kile alichokisema kuwa hajafika ofisini.
Ikumbukwe Mara ya mwisho gavana Lonyang’apuo alihutubia wanahabari mnamo Disemba tarehe 16, kwenye mkutano uliofanyika kwenye wadi ya Tapach ambapo alikuwa akisambaza ng’ombe wa kisasa wa maziwa kwenye kaunti.