WENYEJI WA ENEO LA MOIBEN KAUNTI YA TRANS NZOIA KUNUFAIKA NA HUDUMA ZA SERIKALI BAADA YA SERIKALI KUTWAA ARDHI YENYE EKARI 150


Serikali kuu imefanikiwa kutwaa ardhi yenye ekari 150 katika eneo la Moiben Nzoia katika eneobunge la Cherangany kaunti ya Trans Nzoia iliyonyakuliwa zaidi ya miongo miwili iliyopita na familia ya bwenyenye ambayo pia ina ushawishi mkubwa serikalini.
Akiwa ameandamana na masoroveya wa serikali mwakilishi wa wadi ya Motoshiet kwenye kaunti hiyo Benard Aliang’ana amesema kuwa huduma za serikali sasa zitapigwa jeki katika eneo hilo akisema kuwa wakaazi wa eneo hilo wamekuwa wakihangaika kusaka huduma za afya, elimu ya vyuo vya kiufundi na huduma za usalama kutokana na ukosefu wa kituo cha polisi.
Aliang’ana kadhalika ametoa wito kwa wizara ya ardhi na tume ya kitaifa ya ardhi NCL kuhakikisha kuwa inathibitisha umiliki wa ardhi kabla ya kutoa hati miliki akisema kuwa mizozo ya umiliki wa ardhi imekuwa kizingiti kwa utekelezaji wa miradi ya maendeleo.