Wazee walalamikia kucheleweshwa mgao wao

Baraza la wazee katika kaunti ya Pokot Magharibi,Picha/Maktaba

Na Benson Aswani,
Baraza la wazee katika kaunti ya pokot magharibi wamelalamikia kucheleweshwa fedha ambazo zinatolewa kwa ajili ya wazee.


Wakiongozwa na mwenyekiti wa baraza hilo katika wadi ya Tapach Julius Lokudia, wazee hao walisema kwamba tangu serikali ya sasa kuingia mamlakani, hawajakuwa wakipokea fedha hizo jinsi ilivyokuwa katika serikali iliyotangulia.


“Serikali iliyotangulia ilizindua hizo fedha ila tangu serikali ya sasa kuchukua uongozi, imekuwa vigumu sana kuzipata. Kwa hivyo tunaomba serikali kuhakikisha kwamba fedha hizo zinawafikia wazee,” alisema Lokudia.


Aidha wazee hao walitoa wito kwa serikali kuongeza fedha hizo hadi shilingi alfu tano wakisema kwamba pesa ambazo wanapewa sasa hazitoshelezi mahitaji yao.


“Tunaomba serikali kuongeza pesa hizo zifike alfu 5 ili ziweze kutusaidia. Kiasi ambacho tunazopewa sasa ni kidogo mno,” alisema.


Wakati uo huo wazee hao walitaka mbinu ya kutumwa fedha hizo kwa wazee kubadilishwa kwani mbinu inayotumika kwa sasa ya kupitia kwa simu au benki inawagharimu pakubwa.


“Mbinu ambayo imekuwa ikitumika ya kupeana fedha hizo kwa wazee inatugharimu sana. Wengi wetu tunalazimika kuuza mbuzi kuja kuchukua fedha hizo. Kwa hivyo tunaomba serikali kuzileta fedha hizo hadi maeneo ya mashinani ili wazee wazipate kutoka sehemu wanazoishi,” aliongeza.