WAZAZI WATAKIWA KUWACHUNGA WATOTO WAO MSIMU HUU WA LIKIZO NDEFU WAKIWA NYUMBANI KWA ZAIDI YA MAJUMA SABA


Shule zikiwa zimefungwa rasmi kwa ajili ya likizo ya muhula wa tatu, wito umetolewa kwa wazazi na jamii kwa jumla kuwa makini na wanafunzi na kuhakikisha kuwa wanasalia salama ikizingatiwa watasalia nyumbani kwa kipindi kirefu cha majuma saba.
Mkurugenzi wa elimu eneo la Kipkomo kaunti hii ya Pokot magharibi Evans Onyancha amewataka wazazi kufuatilia mienendo ya wanao na kuhakikisha wanafahamu kila hatua wanayopiga ili warejee shuleni wakiwa katika hali nzuri shule zitakapofunguliwa.
Onyancha amewataka wazazi na walezi kutowaruhusu wanao kujihusisha na maswala ambayo huenda yakawaathiri na badala yake kuwahusisha zaidi katika maswala ya elimu.
Wakati uo huo Onyancha amesema kuwa maandalizi kwa ajili ya mitihani ya kitaifa kwa darasa la nane na kidato cha nne ambayo inatarajiwa kuanza juma lijalo yamekamilika huku akitoa hakikisho la mitihani hiyo kufanyika katika njia salama na kutoripotiwa kwa visa vyovyote vya wizi.
Amesema kuwa wanafunzi kutoka shule ambazo hazina idadi inayohitajika watalazimika kufanyia mitihani yao katika shule zingine ili kuafiakia idadi ya wanafunzi 30 inayohitajika kulingana na sheria za baraza la mitihani KNEC.