WAZAZI WATAKIWA KUWA KARIBU NA WANAO SHULE ZINAPOTARAJIWA KUFUNGWA .

Muhula wa tatu unapokaribia kukamilika miito imeanza kutolewa kwa wazazi katika kaunti ya Pokot magharibi kuwatunza vyema wanao katika muda wa takriban miezi miwili watakayokuwa nyumbani baada ya shule kufungwa.

Msimamizi wa kitengo cha elimu katika shirika la Finn church aid Lilly Chepchumba alisema kwamba huu ndio msimu ambao tamaduni mbali mbali hutekelezwa kwa wingi ikizingatiwa kipindi ambacho watoto watasalia nyumbani, akiwataka wazazi kujitenga na tamaduni ambazo huenda zikaathiri elimu ya wanao.

“Watoto watafunga shule mwezi huu na watakuja kukaa na wazazi kwa angalau miezi miwili. Ombi langu kwa wazazi ni kwamba tuwachunge hawa watoto hasa wakati huu na kutowahusisha katika tamaduni zilizopitwa na wakati za ukeketaji pamoja na ndoa za mapema, ili shule zinapofunguliwa waweze kurejea shuleni wakiwa katika hali nzuri.” Alisema Chepchumba.

Akizungumza mjini Makutano, Chepchumba aidha alitoa wito kwa wazazi kutekeleza kikamilifu wajibu wao wa ulezi kwa kuwa karibu na wanao na kuangazia changamoto ambazo huenda wakapitia ili kukuza kizazi kijacho chenye maadili.

“Nawasihi wazazi wetu kwamba tukumbuke watoto ni jukumu letu. Wanapokumbwa na matatizo hasa yanayohusu msongo wa mawazo tuwakaribie na tuwasikilize, ili tuweze kukuza kizazi cha kesho ambao watoto wetu watakuwa wa manufaa katika jamii.” Alisema.

Wakati uo huo chepchumba aliwataka watoto kutokubali kuhusika tamaduni za ukeketaji au kuozwa mapema na badala yake kutafuta msaada wa idara husika iwapo watashinikizwa na jamaa zao kuhusika vitendo hivyo.

“Nina ombi pia kwa watoto. Mnapokumbwa na changamoto pengine mzazi anataka ukeketwe au kukuoza mapema, kimbia haraka hadi kwa chifu au maafisa wa watoto ili tuweze kukuza jamii ambayo inalinda haki za watoto.” Alisema.