WAZAZI WATAKIWA KUTOKUWA NA HOFU WANAO WANAPOREJEA SHULENI.


Wanafunzi wakiendelea kuripoti shuleni baada ya kufunguliwa shule kwa muhula wa kwanza baadhi ya shule kaunti hii ya pokot magharibi zimetangaza kuweka mikakati kabambe kudhibiti maambukizi ya virusi vya corona hasa ikizingatiwa ni mara ya kwanza kwa wanafunzi wote kurejea shuleni tangu kuripotiwa janga la covid 19 nchini.
Mkurugenzi wa shule ya binafsi ya Makutano central mjini makutano kaunti hii ya pokot magharibi Wilbert Mukhwana amesema kuwa shule hiyo ina vifaa vya kutosha kuhakikisha kuwa kanuni zote za kukabili maambukizi ya virusi vya corona zinazingatiwa akieleza imani kuwa wanafunzi watakuwa salama.
Aidha Mukhwana amesema kuwa nusu ya walimu wa shule hiyo wamepokea chanjo dhidi ya virusi vya corona huku akitoa wito kwa walimu ambao hawajapokea chanjo hiyo kufanya hivyo ili kuhakikisha usalama wa wanafunzi wakiwa shuleni.
Amewahakikishia wazazi kuwa wanao watakuwa salama na kupokea huduma inayostahili huku pia akitoa wito wa ushirikiano kupitia kulipa karo kwa wakati ili kufanikisha shughuli za masomo na maswala mengine shuleni humo hasa kipindi hiki cha janga la corona.