WAZAZI WATAKIWA KUSHUGHULIKIA HALI YA WANAO KUTUMWA NYUMBANI KILA MARA KARO.

Wazazi katika kaunti hii ya Pokot Magharibi wameshauriwa kushirikiana na uongozi wa shule ili kuhakikisha kuwa wanao wanasalia shuleni na kuendeleza shughuli za masomo.

Ni wito wake mwenyekiti wa bodi ya elimu katika kaunti hii ya Pokot magharibi Abraham Ruto ambaye amesikitikia hali kwamba wengi wa wanafunzi wamekuwa wakirejeshwa nyumbani kutafuta karo siku tatu tu baada ya shule kufunguliwa rasmi kwa muhula wa tatu.

Akizungumza na kituo hiki Ruto amewataka wazazi kuhakikisha kuwa wanao wanashughulikiwa hasa ikizingatiwa kwamba muhula huu ni mfupi mno na kwamba si wakati wa mwanafunzi yeyote kuwa barabarani kila mara hasa ikizingatiwa ni muhula ambapo mitihani ya kitaifa inaandaliwa.

“Watoto wengi wapo barabarani kutokana na tatizo la karo nawaomba wazazi tushirikiane na walimu wetu ili tuweze kuchangia matumizi katika shule na watoto waendelee na masomo kwa kuwa muhula huu ni mfupi mno na pia tuna mitihani ya kidato cha nne darasa la nane na gredi ya sita.” Alisema.

Amewataka wazazi kutumia chochote walicho nacho kugharamia karo ya wanafunzi au kuelewana na uongozi wa shule husika kuhusu jinsi watakavyolipia karo ya wanao ili kuhakikisha wanasalia shuleni.

“Si lazima karo iwe katika fedha wazazi wanaweza kutumia mapato waliyo nayo kama vile kuni, mboga na waweze kuwasiliana na shule wapeleke kidogo walicho nacho ili wanafunzi wasalie shuleni.” Alisema.

[wp_radio_player]