WAZAZI WATAKIWA KUKUMBATIA MTAALA WA CBC KWA MANUFAA YA WANAO.

Wazazi katika kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kukumbatia mfumo mpya wa elimu CBC kwa manufaa ya wanao siku za usoni.

Akizungumza katika hafla ya elimu katika shule ya msingi ya kibinafsi ya Evergrace viungani mwa mji wa makutano, mshirikishi wa elimu ya msingi ECDE katika wadi ya Mnagei Rose Lochulem alisema kwamba mtaala wa CBC unampa mwanafunzi uwezo wa kujiajiri ikilinganishwa na ule wa 8.4.4.

Aidha Lochulem alisema kwamba ni lazima taifa likumbatie mtaala wa CBC ili kuafikia ruwaza ya mwaka 2030 akisisitiza kwamba dosari ambazo zipo kwenye mtaala huo zinashughulikiwa.

“Huu mfumo wa elimu tulio nao sasa ni wa kuwafunza watoto kutafuta ajira za afisini na sasa hivi kazi hizo hazipo. Tunafahamu kwamba mtaala wa CBC una dosari ila utarekebishwa. Tunafaa kuukumbatia kwa manufaa ya maisha ya baadaye ya watoto wetu kwani hawatategemea kuajiriwa kwani unampa mwanafunzi ujuzi wa kujiajiri mwenyewe.” Alisema Lochulem.

Wakati uo huo Lochulem alitumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi kuwa makini na malezi wanayowapata watoto katika miaka ya kwanza punde baada ya kuzaliwa kwani ni hayo ndiyo yatategemea hali ya mtoto katika miaka yake ya baadaye.

“Nawahimiza wazazi kuwa waangalifu sana na malezi ambayo wanawapa watoto wao hasa miaka ya kwanza kwa sababu hali na maisha yao ya baadaye hutegemea pakubwa na jinsi ambavyo wametunzwa katika miaka yao ya mwanzo wanapozaliwa.” Alisema.