WAZAZI WATAKIWA KUKUMBATIA ELIMU KWA WANAO KAMA NJIA MOJA YA KUKABILI WIZI WA MIFUGO.
Wito umetolewa kwa wazazi katika kaunti ya Pokot magharibi kuchukulia kwa uzito swala la kuhakikisha kwamba watoto wao wanapata elimu kama njia moja ya kukabili tatizo la utovu wa usalama ambao unasababishwa pakubwa na wizi wa mifugo.
Akizungumza katika kikao na wadau mbali mbali katika mkahawa wa Horizon kwenye makutano ya Tartar, waziri wa utumishi wa umma kaunti hiyo Martine Lotee alisema kwamba iwapo wakazi watakumbatia elimu kwa wanao, hakutakuwa na mtu yeyote ambaye atawazia kushiriki wizi wa mifugo.
Alisema serikali ina mpango wa kujenga shule hasa za mabweni katika maeneo ya mipakani kama sehemu ya mikakati ya kuwazuia vijana kuwa katika mazingira ambayo yatawapelekea kuwazia kujihusisha na maswala ya kihalifu.
“Jambo la muhimu ni kuwapeleka watoto shule. Hao watoto wanaozaliwa wakipelekwa shule tutakosa watu wanaojihusisha na wizi wa mifugo. Serikali inapania kujenga shule katika maeneo ya mipaka na ambazo zitakuwa na mabweni ili watotot wasiwe katika mazingira ya kufikiria kujihusisha na uhalifu.” Alisema Lotee.
Aidha Lotee alisema kwamba serikali ya kaunti inaendeleza mikakati ya kujenga barabara za kiusalama hasa maeneo ambako kunashuhudiwa utovu wa usalama pamoja na kuhakikisha kwamba swala la mtandao linashughulikiwa ili kuimarisha mawasiliano kama njia moja ya kukabili tatizo la usalama.
“Tunataka kufungua barabara za kiusalama maeneo hayo. Na pia kuna tatizo la mitandao katika baadhi ya maeneo ambapo mawasiliano ni tatizo hali ambayo inawapa wakati mzuri wahalifu kuendeleza shughuli zao. Kwa hivyo swala hilo pia liko kwenye mpango.” Alisema.