WAZAZI WATAKIWA KUCHANGIA NIDHAMU MIONGONI MWA WANAFUNZI.


Wazazi katika kaunti hii ya Pokot magharibi wametakiwa kushirikiana na walimu katika kuhakikisha nidhamu miongoni mwa wanafunzi.
Mkuu wa elimu eneo la bonde la ufa Jared Obiero amesema kuwa wazazi ndio walio na jukumu kuu la kuhakiksiha kuwa nidhamu inadumishwa miongoni mwa wanao na wala si kuwaachia walimu pekee hali inayopelekea ongezeko la utovu wa nidhamu miongoni mwao.
Akirejelea visa vya kuteketezwa majengo ya shule ambavyo vilishuhudiwa pakubwa katika shule mbali mbali muhula wa pili, Obiero amesema kuwa ni wazazi ndio hugharamikia pakubwa ukarabati wa majengo hayo hivyo ni jukumu lao kulinda mali ya shule kupitia kutia nidhamu miongoni mwa wanao.
Wakati uo huo Obiero amewataka wazazi kukumbatia mtaala mpya wa elimu wa CBC anaoutaja kuwa bora zaidi ikilinganishwa na ule wa 8.4.4, akiwahakikishia kuwa mikakati ya kutosha imewekwa na serikali kuhakikisha mtaala huo unafanikiwa licha ya changamoto zinazoshuhudiwa.