WAZAZI WAONYWA DHIDI YA KUWANYIMA WANAO ELIMU.


Idara ya usalama kwa ushirikiano na ile ya elimu kaunti ndogo ya kacheliba katika kaunti hii ya Pokot magharibi imeanzisha mikakati ya kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliofanya mtihani wa kitaifa kwa darasa la nane KCPE mwaka huu wanajiunga na kidato cha kwanza.
Naibu kamishina wa Kacheliba Kenneth Kiprop amesema kufikia sasa zaidi ya asilimia 88 ya wanafunzi hao wamejiunga na kidato cha kwanza, ila kwa sasa wanashirikiana na shule mbali mbali eneo hilo kubaini wanafunzi ambao hawajaripoti shuleni ili kuwafuatilia na kuhakikisha wanafanya hivyo.
Kiprop ametaja hali ya umasikini miongoni mwa jamii nyingi eneo hilo kuwa chanzo cha baadhi ya wanafunzi kutoripoti shuleni japo akitoa wito kwa wazazi wa wanafunzi hao kuzungumza na wakuu wa shule husika kuwaruhusu wanao shuleni wakati wanapojitahidi kutafuta karo.
Hata hivyo amewaonya wazazi ambao wanakosa kuwapeleka wanao shuleni kimakusudi kwa lengo la kuwaoza kuwa oparesheni itaanzishwa na watakaopatikana wakiwa na watoto wao nyumbani kwa lengo hilo watakabiliwa kisheria.