WAZAZI WAONYWA DHIDI YA KUSALIA NA WANAO NYUMBANI KUFUATIA KARO.

Katibu wa kaunti ya Pokot magharibi Jonathan Siwanyang amewaonya wazazi dhidi ya kuruhusu wanao kusalia nyumbani kwa sababu ya ukosefu wa karo.

Akizungumza katika hafla moja huko Soak eneo bunge la Kapenguria, Siwanyang badala yake aliwataka wazazi kufanya mazungumzo na uongozi wa shule husika na kuelewana jinsi watakavyolipa karo ili kuwapa nafasi wanafunzi kuhudhuria masomo.

Aidha Siwanyang alisema licha ya kwamba jamii nyingi zinapitia hali ngumu ya kiuchumi, wazazi wanapasa kujizatiti na kuhakikisha kwamba wanalipa karo iliyosalia hasa baada ya serikali ya kaunti kulipa sehemu ya karo hiyo kupitia basari.

“Wakati mzazi unapoacha mtoto akae nyumbani unafikiria nini kuhusu huyo mtoto? Najua kwamba sasa hivi watu wengi wanapitia changamoto za kifedha kufuatia kupanda gharama ya maisha ila hii haipasi kufanya watoto kusalia nyumbani. Kunapasa kuwa na maelewano baina ya mzazi na mwalimu mkuu kuhusu jinsi ya kulipa karo ili kumruhusu mwanafunzi kusalia shuleni.” Alisema Siwanyang.

Wakati uo huo Siwanyang aliwataka wakuu wa shule kushirikiana na machifu kuhakikisha kwamba wanafunzi ambao wanasalia nyumbani wanarejeshwa shuleni ili waendeleze masomo yao sawa na wanafunzi wengine.

“Walimu wakuu tushirikiane na machifu ili kuhakikisha kwamba wanafunzi ambao labda wanasalia nyumbani wanarejeshwa shuleni ili pia wapate kusoma kama wanafunzi wengine.” Alisema.