WAZAZI WALAUMIWA KWA UTOVU WA NIDHAMU MIONGONI MWA WANAFUNZI.

Na Benson Aswani
Huku visa vya wanafunzi kuchoma shule vikizidi kushuhudiwa kote nchini viongozi wa kidini wamelaumu wazazi kutowapa wanao ushauri nasaha na mwongozo bora katika maisha mbali na kutohudhuria mafunzo kanisani.
Wakiongozwa na Katibu mwekahazina wa kitaifa katika Kanisa la CBM Kenya James Mijuanda viongozi hao wamekashifu vikali uchomaji huo wa mabweni akisema ipo haja ya ushirikiano wa wazazi, kanisa na serikali kutoa mwongozo bora na ushauri kwa wanafunzi ili kuepukana na visa vya utovu wa nidhamu kwa wanafunzi wakiwa shuleni.
Ni matamshi yaliyoungwa mkono na mchungaji wa kanisa hilo Vitalis Onyando akisema hulka hiyo imetokana na wazazi kuwatelekeza na kutokuwa karibu na wanao wanapokuwa likizoni ili kufuatilia tabia na mienendo ya wanao pamoja na hatua ya serikali kulazimisha wanafunzi wote waliofanya mtihani wa darasa la nane kujiunga na shule za upili bila kuzingatia uwezo wa mwanafunzi.