Wazazi wahimizwa kuwekeza katika elimu ya wanao

Kina mama katika kaunti ya Pokot magharibi,Picha/Benson Aswani

Na Emmanuel Oyasi,
Kina mama katika kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kuwa msitari wa mbele kukumbatia elimu kwa ajili ya wanao hasa wa kike na kujitenga na tamaduni iliyopitwa na wakati ya ukeketaji.


Akizungumza jumatatu baada ya kukabidhi kundi moja la kina mama eneo la Swam eneo bunge la Kacheliba hundi ya shilingi alfu 510, mwakilishi kina mama kaunti hiyo Rael Aleutum alisema ukeketaji una athari kubwa kwa afya ya mtoto na ni wakati jamii inapasa kujitenga nao kabisa.


“Ningependa kuwahimiza kina mama kwamba, tuwapeleke shule wasichana wetu na kuwatenga na tamaduni ya ukeketaji ambayo imepitwa na wakati, na ambayo ni hatari sana kwa afya yao,” alisema Bi. Aleutum.


Ni hatua ambayo ilipongezwa na viongozi walioandamana na Aleutum wakiongozwa na mwakilishi wadi mteule Mary Mulee ambao walitoa wito kwa serikali kuongeza mgao kwa afisi ya mwakilishi kina mama ili kuyawezesha makundi zaidi ya akina mama.


“Serikali inapasa kuongeza kiwango cha fedha ambacho kinatengewa afisi ya mwakilishi kina mama, kwa sababu majukumu ambayo wanatekeleza ni mengi sana. Pesa ambazo wanapokea kwa sasa hazitoshi,” alisema Mulee.


Wakati uo huo Aleutum alitumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi kuwapeleka wanao shuleni wakati huu ambapo shule zimefunguliwa kwa muhula wa pili, na kuhakikisha wanasalia shuleni ili watimize ndoto zao maishani.


“Nawahimiza pia wazazi kwamba tuwapeleke watoto wetu shule wakati huu ambapo shule zimefunguliwa na tuhakikishe kwamba wanasalia darasani ili wafanikishe ndoto zao maishani,” alisema.