WAZAZI WA SHULE YA UPILI YA ST COMBONI WATAKIWA KUWAREJESHA WANAO SHULENI.


Wazazi wa wanafunzi wa shule ya upili ya wavulana ya St Comboni eneo la Alale kaunti hii ya Pokot magharibi wametakiwa kuhakikisha kuwa wanao wanarejea shuleni baada ya kukamilika likizo fupi ambayo ilikamilika siku ya jumatatu juma hili.
Kulingana na OCPD wa eneo hilo Nathan Sanya wanafunzi wa shule hiyo waliondoka shuleni humo juma jana bila ruhusa ya mwalimu mkuu, na hadi kufikia sasa hawaja ripoti shuleni licha ya kukamilika likizo hiyo katika kile amesema tofauti kati yao na mwalimu mkuu wa shule hiyo.
Sanya ameelezea hofu kuwa huenda hali hii ikaathiri matokeo yao katika mitihani ya kitaifa ikizingatiwa shule hiyo haikufanya vyema katika mtihani wa mwaka huu, akisema ni vyema wanafunzi hao kufika shuleni ili kuwasilisha malalamishi yao kwa wadau husika.
Amewataka wazazi wa wanafunzi hao kutowashikilia wanao nyumbani ila kuhakikisha wanarejea shuleni, kwani maafisa wa elimu wamepiga kambi katika shule hiyo ili kubaini chanzo cha wanafunzi hao kuondoka shuleni bila idhini rasmi.