WAZAZI POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUTILIA MAANANI ELIMU KUWA SULUHU KWA UTOVU WA USALAMA.


Wito umetolewa kwa wakazi wa kaunti ya Pokot magharibi kukumbatia elimu kwa ajili ya wanao na kuhakikisha kwamba wanasalia shuleni kwa kuwajibikia mahitaji yote kwa manufaa yao ya siku za usoni.
Ni wito wake naibu kamishina eneo la pokot ya kati Jeremiah Tumo ambaye alisema kwamba ni kupitia elimu ambapo nyingi ya changamoto ambazo zinakabili jamii kama vile vijana kujiunga na makundi ya kihalifu zitapata suluhu.
Tumo alisema wadau mbali mbali wamewekeza raslimali za kutosha katika kuhakikisha mazingira bora kwa wanafunzi na hivyo wazazi wanapasa kutumia fursa hiyo kuhakikisha kwamba wanao wanapata elimu.
“Mashirika mbali mbali yasiyo ya serikali yamejitolea kuimarisha mazingira ya wanafunzi kaunti hii ikiwa ni pamoja na kujenga madarasa, kuleta maji shuleni na mambo mengine mengi. Hivyo nawaomba wazazi watumie nafasi hii kuwapeleka wanao shuleni. Ni kupitia kwa wanao kupata elimu tu ndipo tutakabili hali ya vijana kujihusisha na makundi ya kihalifu.” Alisema Tumo.
Wakati uo huo Tumo alitoa wito kwa wadau kumwangazia zaidi mtoto wa kiume katika jamii akisema kwamba kwa muda mrefu mtoto msichana amepewa kipau mbele huku yule wa kiume akipuuzwa hali ambayo imechangia idadi ya wavulana shuleni kupungua pakubwa.
“Kwa muda sasa mtoto wa kike ameangaziwa zaidi hali ambayo imepelekea idadi yao kuongezeka shuleni. Lakini tumemsahau sana mtoto wa kiume. Kwa hivyo wito wangu kwa wadau ni kwamba tumwangazie pia mtoto wa kiume ili pia apate haki ya kupata elimu kama wenzao wa kike.” Alisema.