WAZAZI POKOT MAGHARIBI WATAKIWA KUTAMBUA UMUHIMU WA ELIMU KWA AJILI YA WATOTO WAO.
Wazazi katika kaunti ya Pokot magharibi wametakiwa kukumbatia elimu kwa ajili ya wanao kwa manufaa ya siku zao za usoni.
Ni wito wake mkurugenzi wa elimu kaunti hiyo Simon Wamae ambaye amesema wengi wa wazazi wameendelea kukumbatia tamaduni zilizopitwa na wakati ikiwemo ukeketaji na ndoa za mapema hali ambayo imefanya wengi wa watoto kukosa kuhudhuria masomo.
Hata hivyo wamae amelipongeza shirika la UNICEF ambalo limekuwa likiendeleza mradi wa out of school children akisema kupitia mradi huo shirika hilo limeweza kuwarejesha shuleni idadi kubwa ya wanafunzi ambao walikuwa wamesusia masomo.
“Tumekuja kugundua kwamba wazazi wengi kaunti hii hawatilii maanani alimu ya wanao. Kutokana na hilo wanafunzi wengi wanakaa nyumbani. Ila kupitia mradi huu wa out of school children ambao unafadhiliwa na UNICEF tumeweza kuwarejesha wanafunzi wengi shuleni.” Alisema Wamae.
Wamae alitumia fursa hiyo kuwahimiza wazazi kuhakikisha kwamba wanao wanarejea shuleni baada ya shule kufunguliwa kwa muhula wa tatu kwani serikali tayari imesambaza chakula katika shule zote kuhakikisha kwamba shughuli za masomo haziathiriki kufuatia makali ya njaa.
“Nimesikia baadhi ya wazazi wakisema kwamba sababu ambayo inawafanya kutowapeleka watoto wao shuleni ni ukame ambao umesababisha njaa. Lakini serikali imetoa chakula kwa shule zote na sasa njaa isiwe kisingizio cha wazazi kutowapeleka watoto wao shuleni kwani sasa kuna chakula cha kutosha kwa wananfunzi.” Alisema.