WAZAZI BONDE LA KERIO WATAKIWA ‘KUMKUNJA SAMAKI ANGALI MBICHI’ KATIKA KUKABILI TATIZO LA USALAMA.
Ipo haja kwa wazazi katika kaunti za bonde la kerio kuwa karibu na wanao hasa wa kiume kuanzia umri wao mdogo na kuwapa mwelekeo kuhusiana na hali ya maisha pamoja na kuwafunza maadili ili kukabili uhalifu ambao unashuhudiwa katika kaunti hizi.
Haya ni kwa mujibu wa askofu wa kanisa la AIC kaunti ya Pokot magharibi David Kaseton ambaye alisema kwamba msingi ambao wanapewa watoto katika miaka yao ya mwanzo ni muhimu sana na ndio utakaoamua mkondo ambao watachukua katika maisha yao ya baadaye.
Aidha Kaseton alitaja elimu kuwa swala muhimu kwa maisha ya watoto na kusisitiza haja ya wazazi kuitilia maanani kwa manufaa yao ya baadaye, kwani kwa kufanya hivyo hawatapata muda wa kuwazia kujihusisha na makundi ya kihalifu.
“Wakati umefika ambapo tunahitaji kubadilika. Na mabadiliko haya ni kwanza kuwa karibu na watoto wetu katika umri wao mdogo na kuwafundisha kwamba hamna haja ya kushika bunduki na kwenda msituni. Tuwafunze kuhusu umuhimu wa elimu na kula jasho lao wenyewe.” Alisema Kaseton.
Kaseton aliwataka wadau wote katika kaunti ya Pokot magharibi kuchangia katika juhudi za kuhakikisha kwamba visa vya wizi wa mifugo haviripotiwi miongoni mwa jamii ya Pokot, ili kumaliza dhana kwamba tabia hii huendelezwa na watu kutoka jamii hii.
“Nawaomba wazazi, viongozi na wadau wote tupinge tabia ya wizi kwa kuwa tungependa kukaa kwa amani na majirani zetu. Tunafaa kumaliza dhana kwamba wapokot ndio wanaoendeleza wizi wa mifugo.” Alisema.