WAUMINI WA KIISLAMU POKOT MAGHARIBI WAPOKEA MSAADA WANAPOADHIMISHA EID UL FITR

Waumini wa dini ya kiislamu kaunti hii ya Pokot magharibi wamepokea msaada wa chakula kutoka viongozi mbali mbali kaunti hii wanapokamilisha mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhan hii leo.

Akiwasilisha msaada huo kutoka kwa seneta wa kaunti hii ya Pokot magharibi Samwel Poghisio pamoja na aliyekuwa naibu gavana Nicholas Atudonyang kwa waumini hao katika msikiti wa Makutano, mwakilishi wa wawili hao Hezron Mnang’at amewapongeza waumini hao kwa utulivu wao katika kipindi kizima cha mfungo huo wa mwezi mtukufu wa ramadhan.

Waumini hao kupitia mshirikishi wa baraza la waislamu SUPKEM kanda ya rift valley ambaye pia ni mwenyekiti wa baraza hilo kaunti ya Pokot Magharibi haji Jumbe Omar wamewapongeza viongozi wote ambao wamewapa msaada msimu huu akiwemo gavana John Lonyangapuo pamoja na spika Catherine Mukenyang huku akitoa wito kwa wahisani zaidi kutoa msaada huo.

Wakati uo huo Jumbe amewataka waumini wote wa dini ya kiislamu katika kaunti hii kuhakikisha kuwa wanazingatia kanuni zote za wizara ya afya kukabili maambukizi ya corona wanaposherehekea siku ya kukamilisha mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhan.