WATU WAWILI WAUAWA KWENYE UVAMIZI KAMOLOGON

Taharuki imeendelea kukumba kijiji cha Kamologon mpakani pa kaunti ya Pokot magharibi na kaunti jirani ya Elgeyo marakwet baada ya majangili wanaoshukiwa kutoka kaunti jirani kuvamia kijiji hicho na kuwaua watu wawili wa jamii ya Pokot huku wakitoweka na zaidi ya mifugo 500.

Akithibitisha kisa hicho kamishina wa kaunti ya Pokot magharibi Apolo Okello alisema kwamba uvamizi huo wa jumatatu adhuhuri ulishuhudia ufyatulianaji mkali wa risasi na kupelekea pia watu kadhaa kujeruhiwa.

Alisema kwamba maafisa wa polisi wametumwa eneo hilo ili kudhibiti hali.

“Kuna watu ambao walivamia kijiji cha Kamologon wakawaua watu wawili na kisha kutoweka za zaidi ya mifugo 500. Tumewatuma maafisa wa polisi eneo hilo kusaidia katika kuhakikisha utulivu unarejea.” Alisema Apolo.

Chifu wa Muino Emmanuel Chesta alisema vijana hao wenye umri wa miaka 22 na 18 mtawalia walikuwa wakilisha mifugo eneo hilo kabla ya kukumbana na mauti.

Alisema wavamizi hao walitoweka na kondoo 500, mbuzi 50 na ng’ombe 60 na kuwaelekeza eneo la Kipchumwo marakwet mashariki.

Chesta alisema wavamizi hao walivamia kijiji hicho majira ya asubuhi na kukizingira kwa muda, hali iliyowafanya wakazi kuanza kuyahama makazi yao kwa kuhofia usalama.

“Hawa wavamizi walikizingira kijiji hiki asubuhi ambapo wakazi walianza kuhofia usalama na kisha kuanza kuhama.” Alisema.