WATU WAWILI WANAENDELEA KUPOKEA MATIBABU KATIKA HOSPITALI YA KIMISHENI YA ORTUM BAADA YA KUFYATULIWA RISASI

POKOT MAGHARIBI


Wasiwasi umewakumba wakazi wa Chepkokogh kwenye kaunti ya Pokot Magharibi baada ya watu wawili wa jamii ya Pokot kuvamiwa na kufyatuliwa risasi na watu wanaoaminika kutoka kaunti jirani ya Elgeyo Marakwet.
Kwa sasa wawili hao wanauguza majeraha mabaya katika hospitali ya Misheni ya Ortum huku wakazi wa maeneo hayo wakitoa wito kwa wizara ya usalama wa ndani ya nchi kuingilia kati na kuwasaka wahalifu hao ambao wamedaiwa kutorokea misitu iliyoko mipakani pa kaunti hizo mbili.
Were Simiyu ambaye ni naibu kamishna wa eneo la Sigor amethibitisha kisa hicho.
Haya yamejiri miezi mitatu baada ya watu watatu wakiwamo wanafunzi wawili kuvamiwa na kuuliwa kwa risasi katika eneo hilo.
Ikumbukwe mshirikishi wa maswala ya usalama katika ukanda wa bonde la ufa George Natembeya amekuwa akiendeleza misururu ya mikutano ya amani mipakani pa kaunti za Baringo, Turkana, Pokot na Elgeiyo Marakwet lakini joto la uvamizi halijazimwa kabisa katika maeneo hayo suala ambalo inafaa serikali kulichukulia kwa uzito zaidi.