WATU WAWILI WAJERUHIWA KUHUSIANA NA SIASA ZA ‘WILBARO’ POKOT MAGHARIBI.

NA BENSON ASWANI
Watu wawili wanauguza majeraha katika hospitali ya kapenguria kaunti hii ya Pokot magharibi baada ya kuvamiwa kwa mshale kwa kudaiwa kung’oa wailbaro zilizokuwa zimetundikwa karibu na kalbu ya 442 mjini makutano kwa maandalizi ya ziara ya naibu rais William Ruto kaunti hii.
Kisa cha kuondolewa wailbaro hiyo kinachojiri takriban wiki moja tu baada ya kisa kama hicho kushuhudiwa eneo la Chepareria ambapo wilbaro iliyotundikwa eneo hilo iling’olewa na kuteketezwa kisa kilichoshutumiwa vikali na wandani wa naibu rais William Ruto katika kaunti hii.
Chama cha KUP katika kaunti hii ya Pokot magharibi ambacho kimetajwa pakubwa kuhusika na visa hivyo kimekana vikali kuhusika.
Akizungumza katika mahojiano na kituo hiki, mwenyekiti wa chama cha KUP Geofrey Lipale hata hivyo amesisitiza kauli ya gavana wa kaunti hii ya John Lonyangapuo kuwa ni kinyume cha sheria kutundika ishara za vyama kwa sasa hasa wakati huu ambapo kipindi cha kampeni hakijatangazwa rasmi.
Hata hivyo Lipale ameshutumu vikali hatua ya kushambuliwa kwa mshale wakazi wanaodaiwa kuhusika katika kung’oa mnara huo wa wilbaro, akisisitiza kuwa pande husika zinazohisi kudhulumiwa zinapasa kufuata sheria katika kutafuta suluhu.
Ni kauli ambayo imepuuziliwa mbali na mwakilishi wadi mteule Elijah Kasheusheu ambaye amesema kuwa huu ni msimu wa siasa na mwansiasa yeyote ana haki ya kutundika sera zake eneo lolote kujipigia debe.
Hata hivyo Kasheusheu ametoa wito kwa vijana katika kaunti hii kudumisha amani na kutokubali kutumika na wanasiasa kuhujumu juhudi za wenzao.