WATU WAWILI WADAIWA KUPIGWA RISASI NA KUJERUHIWA SARMACH NA MAAFISA WA KDF.

Mbunge wa Sigor kaunti ya Pokot magharibi Peter Lochakapong.

Na Emmanuel Oyasi.

Mbunge wa Sigor kaunti ya Pokot magharibi Peter Lochakapong amelaani vikali kisa cha kujeruhiwa wakazi wawili waliokuwa wakilisha mifugo wao eneo la Sarmach kwa madai ya kukabiliwa na maafisa wa KDF.

Lochakapong aliwasuta maafisa hao katika kile alisema mazoea ya kutumia risasi kuwakabili wakazi wasio hatia kwa kisingizio kwamba wamejihami kwa bunduki, hali hamna hata mkazi mmoja ambaye amekamatwa na maafisa hao akiwa amejihami.

Aidha Lochakapong alidai kwamba maafisa hao wamechochea uhasama miongoni mwa wakazi wa jamii zinazopakana eneo hilo, kwa kuendeleza mauaji ya mifugo pamoja na kuwajeruhi wakazi wasio na hatia badala ya kuwaandama wahalifu.

“Tunalaani sana kitendo hiki kwa sababu si cha kwanza. Kuna visa vingi kama hivi ambavyo vimetekelezwa na maafisa hawa ambao wamekuwa wakisingizia kwamba wale ambao wanachunga ng’ombe wako na bunduki, madai ambayo hayawezi kuthibitishwa kwa sababu hakuna mkazi hata mmoja ambaye amekamatwa na bunduki.” Alisema Lochakapong.

Wakati uo huo Lochakapong aliwataka maafisa hao kutekeleza majukumu ambayo walipelekwa kufanya maeneo hayo, na kuwahusisha viongozi pamoja na wakazi katika kutafuta suluhu kwa tatizo la utovu wa usalama ambao umekuwepo maeneo ya mipakani kwa miaka mingi.

“Hii kazi ambayo maafisa hawa wanafanya si nzuri. Watafute njia mbadala ya kuwakabili wahalifu kwa sababu hawajaafikia mengi katika oparesheni hii. wahusishe viongozi na wakazi kwa swala hili la kutafuta amani.” Alisema.