WATU WATATU WAFARIKI BAADA YA KUFUNIKWA NA MGODI POKOT KUSINI.
Wachimba migodi watatu wameripotiwa kufunikwa na mchanga walipokuwa wakichimba migodi eneo la Murian katika wadi ya Batei eneo bunge la Pokot kusini baada ya kuporomoka mgodi huo.
Kulingana na Jackson Lomuk mmoja wa wakazi ambao wanaendeleza juhudi za kuwaokoa waathiriwa hao mgodi huo uliporomoka na kuwafunikia ndani tatu hao japo kufikia sasa ni mwili wa mtu mmoja pekee ambao umeopolewa na kuwa wakabiliwa na hali ngumu kuokoa watu wawili ambao wamekwama katika mgodi huo kutokana na kuendelea kuporomoka mgodi wenyewe.
Amesema uwezekano wa kuwapata wawili hao wakiwa hai ni finyu mno ikizingatiwa wamesalia katika mgodi huo tangu jana, akitoa wito kwa mamlaka husika kufika eneo hilo ili kusaidia katika juhudi za kuondoa waliokwama katika mgodi huo.
Lomuk ambaye pia ni daktari ametoa wito kwa wakazi wa eneo hilo kuchukua tahadhari ya juu wanapotekeleza shughuli ya uchimbaji migodi na hata ikiwezekana kujiepusha na shughuli hiyo ili kuepuka maafa zaidi.