WATU WATANO WAUA KATIKA SHUMBULIO LA HIVI PUNDE KIJIJI CHA LAMI NYEUSI POKOT MAGHARIBI.

Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameshutumu vikali mauaji ya watu watano eneo la lami nyeusi mpakani pa kaunti hiyo na kaunti jirani ya Turkana na ambayo yanaaminika kutekelezwa na wavamizi kutoka kaunti jirani.

Wakizungumza Alhamisi wakati walipozuru eneo la tukio, viongozi hao wakiongozwa na naibu gavana Robert Komole walimsuta waziri wa usalama Kithure Kindiki kwa kile walidai utepetevu hasa ikizingatiwa kuna maafisa wa usalama ambao wanaendeleza oparesheni ya kiusalama bonde la kerio.

Walimtaka Kindiki kuandaa kikao na viongozi wa kaunti za bonde la kerio ili kupata suluhu ya kudumu kwa tatizo hili ambalo limedumu kwa miaka mingi.

Sijui ni kazi gani ambayo Kindiki anafanya hapa. Hawa wezi wanatokea Kainuk na wanavuka kwa kutumia daraja. Na hii daraja kuna maafisa wa polisi. Sasa kitu ambacho hatuelewi, hawa polisi huwa wapi wakati majangili hawa wanavuka hadi kuwaua raia? Naomba Kindiki aitishe mkutano wa viongozi wa kaunti za bonde la kerio ili tutafute suluhu kwa pamoja.” Alisema Komole.

Kwa upande wake kamishina wa kaunti hiyo Apolo Okelo alisema afisi yake kwa ushirikiano na serikali ya kaunti na afisi ya mbunge wa Sigor wanaendeleza mikakati ya kuhakikisha  kituo cha polisi kinajengwa eneo hilo katika kipindi cha mwezi mmoja ujao, na kutumwa maafisa wa polisi wa kutosha ili kuimarisha usalama.

“Tutashirikiana na serikali ya kaunti pamoja na afisi ya mbunge wa Sigor ili katika muda wa mwezi mmoja tuanze mpangilio wa kujenga kituo cha polisi sehemu hii, na tuweze kuweka polisi wa kutosha ili waweze kuimarisha usalama wa eneo hili.” Alisema Apolo.

Wakazi wa eneo hilo waliwasuta viongozi wa kisiasa kwa kile walidai  kutoa matamshi ya kiholela ambayo yanachochea uvamizi huo, wakitaka serikali kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua.

“Matamshi ya viongozi kutoka maneo haya hasa kaunti jirani ndio yanachochea mzozo miongoni mwa jamii. Serikali inapasa kufanya uchunguzi dhidi ya matamshi ambayo baadhi ya viongozi wamekuwa wakitoa kiholela na kuwachukulia hatua.” Walisema wakazi.

Mapema Alhamisi wavamizi wanaoaminika kutoka kaunti jirani ya Turkana walivamia kijiji cha Lami Nyeusi eneo bunge la Sigor kaunti ya Pokot magharibi na kuwaua watu watano huku wakitoweka na mbuzi 18.