Watu ‘wala watu’ Pokot magharibi

Na Benson Aswani,
Viongozi katika kaunti ya Pokot magharibi wameendelea kushutumu visa vya watoto wenye umri mdogo kutoweka katika njia zisizoeleweka na kisha kupatikana wakiwa wameuliwa.


Wakiongozwa na mbunge wa Sigor Peter Lochakapong, viongozi hao ambao walikuwa wakizungumza katika boma la mshukiwa mmoja ambaye mifupa ya binadamu ilipatikana kwake, wametaka msako kuendeshwa sehemu mbali mbali za kaunti hii wakidai huenda visa hivi vimetapakaa kote.

“Nasikia hawa watu wametapakaa kote kaunti hii. Na kwa sababu tumeelezwa ukweli, wakati tunapowachunguza hawa wanaokaa hapa, hata wale ambao wamekuwa wakija kula watu kutoka Lelan na maeneo mengine ya kaunti hii pia wapatikane na wachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Lochakapong.


Kulingana na naibu kamanda wa kaunti hiyo ya Pokot Magharibi Joseph Yakan, mshukiwa huyo alitoweka baada ya kubaini anachunguzwa.


Hata hivyo Yakan amesema tayari watu 16 wamekamatwa kuhusiana na matukio hayo huku uchunguzi zaidi ukiendelea.


“Mhusika mkuu bado hajakamatwa. Tuna taarifa kwamba huenda ametorokea taifa jirani la Uganda. Ila kufikia sasa tumewakamata washukiwa 16 ambao wanahusishwa na visa vya kupotea watoto, na tutaendelea na uchunguzi zaidi,” alisema Yakan.


Inadaiwa huenda mshukiwa huyo amekuwa akiwakamata watoto na kuwatumia kama kitoweo hasa baada ya kupatikana mifupa ya binadam kwenye boma lake.


Kwingineko takriban wakimbizi 108 wakiwemo watoto wanne raia wa Eritrea wanazuiliwa katika kituo cha Amakuriat kwenye kaunti hiyo ya pokot magharibi.


Kulingana na naibu chifu wa kata ndogo ya Lokitanyal John Sikamoi wakimbizi hao wanadaiwa kutorokea humu nchini kutokana na machafuko yanayoendelea katika taifa hilo.


Inaarifiwa kuwa wakimbizi hao walipitia Uganda katika mji wa Moroto ambapo walifurushwa na maafisa wa polisi na kutelekezwa kwenye msitu mmoja mpakani pa Kenya na Uganda.